Barua rasmi
Ni aina ya barua inayoandikwa kwa madhumuni ya shughuli za kiofisi au rasmi. Shughuli rasmi ni kama vile: kuomba nafasi ya ajira, kuomba radhi kwa kumkosea mtu, kuomba nafasi ya kutembea eneo fulani kama kituo cha redio au kuwataarifu wafanyikazi kuhusu mabadiliko katika kampuni.
Vitu vya kuzingatia unapoandika barua rasmi.
Hivi ndivyo vitu vinapaswa kuwa katika kila barua rasmi:
1. Anwani : barua rasmi huwa na anwani mbili; anwani ya mwandishi na anwani ya mwandikiwa. Anwani ya mwandishi hujumuisha makao ya mwandishi (shule, kijiji, ) , Sanduku la Posta (S.L.P.), Mji na tarehe ambayo barua inaandikwa. Anwani ya mwandikiwa inahusisha hivi: cheo au dhima ya mwandikiwa, sanduku la posta (S.L.P.) na Mji.
2. Anayeandikiwa barua rasmi.
Katika sehemu hii, mtu anayeandikiwa hurejelewa kama: Kwa Bwana au Kwa Bibi.
3. Lengo
Hii ndio sehemu ya tatu katika uandishi wa barua rasmi. Hapa ndipo madhumuni yanapoandikwa kwa ufupi. Kwa mfano:
MINT: KUOMBA KAZI YA UTABIBU.
Aidha, unaweza kutumia YAH, KUH. YAH inamaanisha Yahusu. MINT humaanisha Mintarafu. KUH humaanisha Kuhusu.
4. Utangulizi
Hii ndio sehemu ambayo ndio mwandishi hueleza matakwa yake kwa ufupi.
5. Mwili
Hii ni sehemu ambayo mwandishi hueleza sifa zake, umri, ujuzi wa kazi na tajriba iwapo ni barua kuhusu kuomba kazi ya utabibu. Aidha, mambo mengine ya maana yanatarajiwa kuelezwa hapa japo kwa muhtasari.
6. Aya ya mwisho
Hii ndio sehemu ambayo mwandishi huomba anayeandikiwa kutilia maanani ombi hilo na kumpa nafasi. Hapa aidha, mwandishi hutarajia majibu kutoka kwa mwandikiwa.
7. Hitimisho
Hii ndiyo sehemu ya kutia kikomo hasa katika barua rasmi. Hapa kuna sentensi kama vile: Wako mwaminifu, wasaalam. Aidha, sahihi hufuata halafu jina la mwandishi hutamatisha.
Kwa mfano:
Wako mwaminifu,
£^&l
Kitivo Mwanga.
Comments
Post a Comment